𝐅𝐔𝐑𝐀𝐇𝐀 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐄𝐎 𝐍𝐈 𝐌𝐀𝐍𝐄𝐍𝐎 𝐌𝐀𝐓𝐀𝐌𝐔 𝐘𝐀𝐓𝐎𝐊𝐀𝐘𝐎 𝐊𝐈𝐍𝐘𝐖𝐀𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐊𝐎 𝐌𝐔𝐌𝐄 𝐖𝐀𝐊𝐄
Wataalamu wa mapenzi na hisia za binadamu wanaeleza kuwa wanawake wanaguswa sana kwa maneno kuliko vitendo. Sauti na maneno mazuri ni vitu ambvyo vinawafanya wawe katika wakati mzuri sana kihisia. Wanaume wao wamefahamika kuwa wanavutwa zaidi kwa kuona kuliko kusikia.
Kwa msingi huu basi ni muhimu sana kwa wanaume walio katika mahusiano ya mapenzi kufahamu siri hii juu ya wenza wao wanawake. Ukitaka kuifanya siku ya mpenzi wako nzuri basi zingatia maneno yako na sauti yako iwe katika kiwango kinachofaa.
Yafuatayo ni maneno manne muhimu kuyasema kila siku kwa mkeo na yataleta mabadiliko makubwa katika mahusiano yenu. Maneno haya yanalainisha moyo,yanajenga uaminifu,yanazidisha upendo,yanaponya majeraha ya mapenzi na yanaleta furaha kati ya wapenzi:
1. “𝐰𝐞𝐰𝐞 𝐧𝐢 𝐦𝐰𝐚𝐧𝐚𝐦𝐤𝐞 𝐦𝐳𝐮𝐫𝐢”
Inawezekana uzuri ni sababu mojawapo ya kumuoa au kuwa naye. Basi hakikisha unamkumbusha kila mara. Wanawake wanahitaji sana kuhakikishiwa kuwa ni wazuri na wanavutia. Ni hatari sana kama hufanyi hivi kwa mkeo,nakuhakikishia wanahitaji kusikia maneno haya. Usipomwambia kuna mtu atamwambia barabarani au kazini na hii ni hatari.
Wanawake wasio ambiwa mara kwa mara kuwa ni wazuri huhangaika sana juu ya kubadilisha mavazi yao na vipodozi. Ikibidi wanaweza wakafikia kuvaa mavazi yasiyo na heshima sana kwa mtazamo wa jamii anayoishi. Hii ni katika kutafuta mrejesho kuwa ni mzuri.
2. “𝐔𝐦𝐞𝐩𝐞𝐧𝐝𝐞𝐳𝐚 𝐦𝐩𝐞𝐧𝐳𝐢”
Hili linaendana na la kwanza hapo juu lakini kupendeza sio lazima uwe mzuri. Uzuri unaweza ukawa wa sura,umbo au tabia zake. Kupendeza ni kutokana na mapambo na mavazi ambayo mtu anavaa.
Kama kuna mambo makubwa ambayo yanawachukulia muda mwingi wanawake wengi basi ni urembo hasa wa mavazi,nywele na vipodozi. Wafanya biashara wajanja wanaweka nguvu zao eneo hili – kutoa huduma za wanawake.
Wanawake wanahitaji sana kuonekana wamependeza hasa toka kwa wapenzi wao. Mrejesho huu ni muhimu kwao na kunawafanya wajisikie vizuri ,kujiamini na kujiona wa thamani. Mwambie mkeo kila siku asubuhi akitoka nyumbani au kila mnapotoka pamoja. Mwambie kila akibadilisha aina ya ususi wa nywele zake.
3: “𝐀𝐬𝐚𝐧𝐭𝐞”
Kwa kweli mke ndiye mtendaji wa mambo mengi nyumbani. Hata kama kuna wasaidizi bado kunahitaji uongozi na bila shaka mke ni kiongozi wa yote haya nyumbani kwa walio wengi.
Utakuta nguo ni safi,chakula ki tayari,watoto wameoshwa na kuvalishwa na mengine mengi. Kuna kila sababu ya kusema “asante”.
Asante ina maajabu makubwa kama ikitolewa kwa jinsi inavyostahili na kwa dhati. Kwanza humfanya anayeambiwa ajione wa thamani sana kwako. Pili humfanya anayefanya aongeze bidii kwa yale anayoyafanya.
Hivyo usiache kushukuru kila siku kwa yale mkeo anayoyafanya. Kunawezekana mengine yakawa si mazuri,lakini hakutakosekana zuri la kushukuru.
Mwambie “𝑨𝒔𝒂𝒏𝒕𝒆 𝒎𝒑𝒆𝒏𝒛𝒊” , “𝑨𝒔𝒂𝒏𝒕𝒆 𝒎𝒌𝒆 𝒘𝒂𝒏𝒈𝒖” na maisha yenu yatakuwa mazuri na yenye furaha.
Fanya kwa vitendo pia,mfano nunua hata kitenge tu na umshangaze kwa zawadi. Mwambie “asante kwa kuwa mama mzuri wa watoto wetu” au “Asante kwa kuwa mke mzuri na rafiki mzuri kwangu”.
4: “𝐍𝐚𝐤𝐮𝐩𝐞𝐧𝐝𝐚”
Kupendwa ni mojawapo ya vitu ambavyo binadamu anahitaji sana. Chukulia mtoto mfano,toka tukiwa watoto kupendwa ni kitu kinachohitajika sana na kinapokosekana kuna madhara makubwa yanayotokea ikiwemo mtoto kutojipenda mwenyewe na kutojiona wa thamani. Kwa wanawake halikadharika,japo ni wakubwa tayari lakini kasumba ya utotoni imo bado ndani yetu na mahitaji ni yaleyale.
Ukiangalia vizuri mahangaiko yote ya mwanamke juu ya urembo na mavazi utaona kuwa ni kutaka kuhakikisha kuwa anapendwa. Au kujinyima na kuishi katika mwenendo ambao wewe kama mume unafikiri ni vizuri au jamii inafikiri ni vizuri ni kutaka kuhakikisha kuwa anapendwa. Basi kwa kumtamkia kuwa unampenda mara nyingi kadili utakavyoweza inampa kujiamini kwa jinsi alivyo na kwa yale anayoyafanya.
Kumwambia mkeo kuwa unampenda na kuonyesha kwa matendo kunamfanya naye akupende zaidi.
Neno hili likitumika kwa dhati na sio kusema tu lina maajabu makubwa katika kuboresha mahusiano ya wenza wapendanao.
Fanya kwa dhati na Upendo
Maneno haya manne yana maajabu makubwa kama yakitekelezwa ipasavyo. Kwanza ni muhimu sana ukayasema kwa dhati na kumaanisha toka moyoni. Kunaweza kukawa na mambo yasiyofikia viwango vya kushukuru au kusifia lakini uanaweza ukaanza na yale machache yaliyopo. Baadae utagundua kuwa hata mengine yanarekebishwa na kufanywa kwa uzuri.
Maajabu ya maneno haya ni katika kubadilisha moyo wa mke na tabia na matendo yake. Ukiyatumia kwa kiasi kinachofaa na kwa kuyamaanisha utafanikiwa na utaboresha mahusianao yenu.
𝐤𝐮𝐦𝐛𝐮𝐤𝐚 "𝒌𝒊𝒍𝒊𝒄𝒉𝒐𝒊𝒗𝒂 𝒌𝒊𝒍𝒊𝒑𝒊𝒌𝒘𝒂"

No comments