Simulizi: Rama sehemeu ya kwanza (01)
Simu yangu ilikua inaita, nilishindwa kuipokea kwani nilikua bize katika kuendesha gari, kutokana na mvua kubwa iliyokua ikinyesha pamoja na giza nene niliona kuwa naweza kugonga mtu kama nikiingiza mkono mfukoni na kuchukua simu. Ndiyo kwana nilikua nimenunua gari, sikua hata na miezo miwili hivyo nilikua bado sijapata uzoefu, niliendesha taratibu huku nikichanganywa na milio ya honi ya magari yaliyokua nyuma yangu, waliniona kama vile nimesimama.
Sikuwajali akili yangu ilielekea mbele tu, nilijifanya siwasikii kwani hata hivyo mvua ilikua kubwa kuwasikia vizuri. Pamoja na mikiki mikiki yote lakini nilifanikiwa kufika nyumbani, bado nilikua sijaweka Geti hivyo niliingiza gari sehemu ambayo naipaki, nikawaka alam kisha nikaingia ndani, mvua ilikua imepungua kidogo ingawa kitendo cha kushuka kwenye gari mpaka kuingia ndani tayari nilikua nimeloana. Nilijibanza pembeni ya mlango, nilitoa funguo ili kufungua mlango.
Nilijua mke wangu atakua ndani lakini sikutaka kumsumbua, alishanikatza mtindo wa kuwagongea, pamoja na kuwa na binti wa kazi lakini mke wangu alikua hataki kabisa kama nikichelewa kutoka kazini nikamgongea. Alinipa funguo hivyo kila nikichelewa basi nakua najifungulia mwenyewe, naingia ndani na kwenda jikoni kuangalia kama kuna chakula wamenibakizia, nakula na kupanda kitandani kimya kimya bila kumbughudhi.
Yeye hapendi kelele hivyo kama ikitokea nikamuamsha basi ugomvi wake ni hakuna kulala usiku mzima. Ili kuepusha shari basi naamua kujiongeza na kujifanyia mambo yangu mwenyewe. Lakini wakati naingiza ufunguo mlango ilikua haiingii, kuna kitu kilikua kinaizuia funguo, nilishika kitasa na kukishusha chini ili kuangalia ni nini ndipo mlango ulifunguka, funguo za ndani ndiyo zilikua zikizuia funguo zangu kuingia. Mlango ulikua haujafungwa ikimaanisha kuwa mke wangu alikua bado hajalala.
“Kelele nyingine hizi!” Niliwaza wakati naingia ndani, kwangu nikiwa nimechelewa kurudi ilikua ni bora kukuta mke wangu kalala kuliko kumkuta macho. Nilikua nimechoka sana kuweza kuvumilia kisirani chake. Niliingia ndani taratibu, taa ilikua imewashwa, nilimkuta binti wa kazi akiwa kasimama, amembeba mtoto huku akimbembeleza. Mtoto alionekana kama anataka kusinzia lakini nilipoingia alishtuka na kuanza kulia.
“Baba! Umemuamsha tena!” Binti wa kazi aliongea wakati naingia.
“Pole, vipi, hataki kulala?” Nilimuuliza huku nikimsogelea kutaka kumsaidia, lakini nilishtuka na kukumbuka kuwa nilikua nimeloana hivyo niliacha kumchukua na kumuulizia kuhusu mke wangu.
“Dada?” Aliniuliza na mimi.
“Ndiyo yuko wapi?” Binti aliniangalia kwa mshangao kidogo, ni kama alikua anatafuta jibu la kunipa lakini hakua nalo. Niliona kama ananichelewesha hivyo niliingia chumbani nikidhani kama nitamkuta mke wangu akiwa kalala lakini haikua hivyo. Chumba kilikua kitupu, haikua kawaida yake kutoka kwa kipindi kile.
Baada ya kujifungua mke wangu alikua ni mtu wa kutulia nyumbani, ndiyo kwanza mtoto alikua na mwezi mmoja na nusu. Nilitoka na kumuuliza vizuri binti wa kazi.
“Alitoka tangu mchana hajarudi na simu yake haipatikani.” Aliniambia, nilishangaa kwa yeye kutoka tangu mchana, bado tulikua hatujaanza kumlisha mtoto kitu chochote zaidi ya maziwa ya Mama yake, kumuacha mtoto mchanga kwa muda wote ule ilimaanisha kumshindisha njaa, ilikua ni kama saa tano za usiku hivyo nilishangaa kusikia kwamba alitoka tangu mchana.
INAENDELEAA

No comments