Header Ads

Header ADS

Simulizi: Rama sehemu ya tatu (03)

 


Nilikata simu na kuizima kabisa, niliendelea na kazi zangu mpaka jioni, nilirudi nyumbani na sikumkuta tena mke wangu. Mtoto alikua na binti wa kazi, nilimuuliza mke wangu kaenda wapi akaniambia tangu mchana nilipompiga alichukua mabegi yake na kuondoka na rafiki yake akisema kuwa hawezi kuendelea kuishi kwenye nyumba ambayo anapigwa na mwanaume. Nilichanganyikiwa kujua kuwa mtoto alikua hajanyonya tangu mchana, nilijua kabisa kuwa kwa kiburi chake mke wangu hawezi kurudi hivyo anaweza kuniulia mtoto.

Nilimpigia simu lakini hakupokea, nilihangaika sana hakupokea na hata rafiki zake nao hawakupokea. Nilipoona hazipokelewi nilimchukua binti wa kazi na mtoto mpaka kwenye gari, nilienda mpaka kwa yule rafiki yake, nilimkuta mke wangu, kaakaa katulia tena wanapika bila wasiwasi wowote, nilimsalimu na kumuomba kuongea naye.

“Hapana, kama unataka kuongea na shoga yangu utaongea mbele yangu, una mnyanyasa sana!” Rafiki yake aliongea, mimi sikutaka kupaniki, kwa maslahi ya mtoto niliamua kuwa mpole ili kumbembeleza arudi na kukubali kulea mtoto.

“Hapana shemeji haya ni mambo yetu, naomba niongee naye!” Nilijishusha pamoja na hasira nilizokua nazo.

“Kama unaongea basi ongea mbele ya Mage (Sio jina lake halisi) sitaki mambo ya siri, unataka nitoke nawewe ili uanze kunipiga!” Mke wangu alijibu kwa hasira, alijifanya kununa kavimba kama vile nimemfanyia kitu kibaya sana. Kabla sijaongea chochote mtoto alianza kulia, ilikua ni njaa, nilimuomba mke wangu kumnyonyesha lakini aligoma, aliniambia kabisa kuwa naringa na namnyanyasa hivyo nibaki na mwanangu.

Nilibembeleza sana mpaka akakubali kumnyonyesha lakinia alikataa katakata kurudi kwangu.

“Naomba basi kama unaishi hapa mimi nitalilipia kila kitu lakini ubaki na mtoto…” Nilimbembeleza baada ya kuona kuwa hakuna dalili za yeye kurudi kwangu.

“Kwani wakati anakuja kwako alikuja na mtoto, hapana, hapa kwangu hawezi kuishi na mtoto, Shogaa kama unaona una shida ya kulea rudi kwa mume wako mimi siwezi kukulea na bado nikamlea na mwanao!” Rafiki yake aliongea, nilimuangalia mke wangu kwa hasira bila kummaliza, nilitaka kumruukia na kumtandika makofi hata kummaliza lakini nilishindwa, nililazimika kuzuia hasira zangu.

Nilianza kazi ya kubembeleza mpaka mke wangu akakubali kubaki na mtoto kwa masaharti kuwa niwe nampa laki mbili kwa wiki na pia nimuachie gari yangu, kwa wakati huo sikua na namna zaidi ya kukubaliana na matakwa yake, ingawa nilikua na wasiwasi sana lakini sikua na namna, nilikua sina njia nyingine ya kumlea mwanangu. Nilimuacha mke wangu pale pamoja na binti wa kazi ili kumsaidia kulea kwani nilijua kabisa mke wangu hawezi kukaa na mtoto masaa yote.

Kila siku nilikua napiga simu kuulizia hali ya mwanangu, nilikua nikimpigia binti wa kazi kwani mara nyingi mke wangu alikua hapokei simu zangu. Lakini baada ya wiki mbili mke wangu alirudi, alikuja na kuniomba msamaha kuwa anajutia makosa yake hivyo anataka turudiane kama zamani na tulee mtoto wetu. Nilifurahi sana kumuona mke wangu na hasa yeye kuomba msamaha, aliniomba msamaha kwa vitu vingi na matendo mengi ambayo alishanifanyia nyuma.

“Baada ya kukaa mbali na wewe ndipo nimegundua kuwa nakupenda na siwezi kuishi bila wewe.”

Aliniambia huku akilia, nilifarijika sana, sikuweza kuuliza hata sababu ya yeye kurudi, nilikua na amani kiodgo kuwa mwanangu atakua mikononi mwangu na nitaweza kumlea mimi mwenyewe. Tulirudiana na maisha yaliendelea, mke wangu alianza kuwa na nidhamu, hakua akitoka toka tena, alikua kama kaacha pombe, kwa wiki mbili alitulia kabisa. Lakini siku moja rafiki  nikiwa mjini nilikutana na yule rafiki yake, yule yule ambaye alimpokea. Aliponiona ingawa nilitaka kumkwepa lakini alinifuata na bila salamu aliniambia.

“Muambie huyo Malaya wako kama alifikiri nitamuacha mchumba wangu basi amebugi, nimerudiwa na pete nimevalishwa!”

Sikutaka kujua kilichoendelea lakini kama unavyojua mtu mwenye hasira, aliniambia kuwa alimfukuza mke wangu kwake baada ya kumfumania kitandani na mchumba wake.

“Wewe na wewe ni fala tu, mwanamke gani anafanya mapenzi na mwanaume mwingine tena kitandani mtoto wake akiwepo?” Aliongea na kuniambia mambo mengi sana ya mke wangu, niliumia sana lakini sikusema chochote, ilikua ni sehemu ya wazi hivyo nilihoifia kama nikihjibishana naye basi ataropoka na hata kunidhalilisha. Nilimuacha akaongea mpaka akamaliza akaondoka zake.

Nilirudi nyumbani nikiwa na hasira sana, niliumia kuwa mke wangu hakurudi kwakua kajutia makosa yake bali alirudi kwakua kafumaniwa na hakua na sehemu nyingine ya kwenda. Niliumia sana, nilijaribu kuficha hisia zangu lakini nilishindwa, niliamua kumuuliza mke wangu sababu ya kuja kwangu. bado alisisitiza kuwa alirudi kwaajili ya mapenzi, niliamua kumuambia ukweli kuwa nimekutana na rafiki yake na kaniambia kila kitu. Aliruka futi mia kisha akanigeuzia kibao kuwa mimi ndiyo natembea na rafiki yake na nina mpango wa kumfukuza ili niishi naye.

“Nilijua muda mrefu kuwa una mtaka nikanyamazia lakini sasa hivi naona mmeamua kukaa ili kunisingizia vitu!” Alijiongelesha sana lakini mimi bado niliendelea na msimamo wangu. Tuligombana sana akanuna hukua kiniambia kuwa kama nimemchoka basi nimuache salama lakini si kumsingizia mambo ya uongo, alianza kulia kama mtoto, sijui kwanini lakini nilianza kumuonea huruma na ingawa mimi nilishawahi kumfumania na yule mwanaume lakini nilianza kama kumuamini na kuhisi labda rafiki yake anamuonea wivu kweli, nilimuomba msamaha mimi lakini hakukubali, alinuna kabisa.

Siku iliyofuata ilikua ni Ijumaa, baada ya Swala niliitwa na Shehe, aliniambia kuwa anataka nibaki. Mke wangu siku hiyo hakuja Msikitini, nikijua ni mambo ya Msikitini kwani mimi ni mmoja wa viongozi Msikiti nilikubali, aliniita mpaka ofisini kwake. Lakini ile naingia nilishangaa namuona mke wangu kakaa na mtoto, alionekana kuvimba macho kama mtu aliyekua analia. Nilishtuka na kuuliza mke wangu alikua anafanya nini pale wakati hata hakuja Msikitini.




RAMA; MAMA YENU AKIRUDI NAOMBA MUMUAMBIE KUWA MIMI NIMETOKA!—SEHEMU YA TATU

“Mume wangu anatembea na rafiki yangu!” Mke wangu aliongea kwa sauti ya kupiga kelele mara tu baada ya mimi kuingia.

“Hapana  Shemeji, hembu tulia, umeshanielezea kila kitu, hembu tulia kwanza tusikilize upande mwingine!” Mke wangu hakutaka kutulia, aliongea maneno mengi ya kunipondea, aliongea jinsi nilivyompiga, hakusema kuhusu kunywa pombe na kumucha mtoto. Kila kitu kilikua ni kunishutumu mimi. Ingawa alishamuambia Shehe kila kitu lakini nilipoingia alirudia tena, kwa hasira huku akilia.

Nilinyamaza tu nikimuangalia kwa mshangao, kwa namna alivyokua anaigiza sikua na neno la kuongea. Hasira zilinipanda na kutaka kuongea kila kitu, lakini kuna kitu kiliniambia.

“Hata ukiongea ni kujidhalilisha tu, mwanaume huwezi kuwa hivyo, hembu kuwa na kifua bwana!” Nilinyamaza kidogo kila nilopokua nikiulizwa nilishindwa cha kujibu.

“Kwahiyo unataka njni? Unataka talaka, kama ni talaka sema hapa mimi niandike, nina kalamu na karatasi!” Hasira zilinipanda, ingawa sikua nimepanga kumuacha mke wangu lakini nilijikuta tu nimachoka,a liyonifanyia ni mengi nilishindwa kuvumilia.

“Hamkuja kuchana hapa, hapa mmekuja kusuluhisha….” Shehe aliongea akininyang’anya kalamu na karatasi kwani nilishatoa na kuanza kuandika. Mke wangu kuona vile nilimuona kabisa ananywea, alianza kutetemeka kwani nilikua nimekasirika kiasi kwamba hata kuongea nilikua naongea kwa kigugumizi. Niliona kama wananizingua, nilitoka nnje kwenda nyumbani kwangu, lakini sikufika, kichwa kilikua cha moto, nilikua nimepaniki sana, nilikua kama mtu aliyechanganyikiwa, sikua na gari siku hiyo, nilijikuta natembea mpaka kwenye Baa moja.

Katika maisha yangu nilikua sijawahi kunywa pombe lakini siku ile nilitamani sana kunywa pombe. Niliagiza bia mbili Safari, nilitaka kuzinwa lakini kila niliposhika chupa kujaribu kuiweka mdomoni niliona picha ya binti yangu, mtoto wangu ambaye bado alikua mchanga.

“Siwezi kuwa kama Mama yake, siwezi kunywa, nikianza kunywa yule mtoto atakufa. Picha ya siku Mke wangu alipomtelekeza na kwenda kwa mwanaume mwingine ilinijia, nilishindwa kunywa, masaa mawili nilikua naziangalia zile bia, nilishindwa kunywa nikatoa noto ya elfu kumi nikampa mhudumu nikaondoka bila hata kudai chenchi.

Nilienda nyumbani na kukuta mke wangu bado hajarudi, sikushangaa nilichukua simu na kuanza kumpigia lakini hakupokea. Nilianza kupaniki kwani nilijua kabisa atakua kaenda kwenye mambo yake, nilihangaika kutafuta marafiki zake lakini hakuna aliyejua alikua wapi? Nilimpigia rafiki yake mmoja ambaye hawakua karibu sana na kumuuliza, kusema kweli sikutegemea jibu lolote lakini nilikua nimepaniki hivyo nilitaka tu kuuliza kila mtu kwani nilikua nishaanza kuchanganyikiwa.

Sijui nini kilitokea lakini alikuta ananishauri kutafuta maziwa ya kopo, alinielekeza vizuri na mimi sikuwaza sana nilienda kununua na kumpa moto kwelia liyapenda. Mke wangu alirudi saa nne usiku na alikua kalewa, kwakua mtoto wangu alikua kashiba amelala sikuhangaika naye kabisa. Hakua amelewa sana, alikua bado anajitambua hivyo alivyoona kuwa simfuatilii alianza kujirudi na kuomba msamaha. Mimi sikusema chochote nilipanda kitandani kulala, nililala mpaka asubuhi, lakini nilipoamka sikumuona mke wangu.

Nilijua kama kawaida kaenda kwenye mambo yake lakini kuangalia pembeni mtoto naye hakuepo, nilitoka nnje nikijua labda wapo lakini Dada wa kazi aliniambia kuwa Mke wangu alimuamsha usiku ili kumuandalia nguo za mtoto. Hakujua wamewenda wapi, nilianza kupiga simu kwa kupaniki. Simu ya mke wangu iliita bila kupokelewa kwa dakika kama tatu, baadaye meseji iliingia.

“Unataka kuniua, mwanaume gani hunisamehi, nimeondoka nimerudi kwetu, nimemchukua mwanangu akikua utakuja kumchukua.”

Meseji iliishia hapo, haikua siku ya kazi hivyo sikua na sehemu ya kwenda, nilimpigia simu Mama yake akaniambia kuwa mwanae alimpigia simu kuwa na mnyanyasa hivyo akamuambia arudi kwani kwao hajaua. Mama mkwe aliongea maneno mengi ya kashfa na kejeli na kuniambia kuwa hajashindwa kumlea mtoto wake hivyo nisimnyanyasie. Nilijaribu kumuelewesha kilichotokea lakini hakuelewa, alikua mkali na alinishutumu sana kwa kumnyanyasa mwanae kisha akakata simu.

Sikua tayari kumuacha mwanangu akateseke na mke wangu, kwa tabia zake nilijua kabisa hawezi kukaa na mwanangu kwa amani. Niliwasha gari na kumchukua Dada kwenda kwa Mama mkwe wangu. Nilipanga kumchukua mwananguhata kwa nguvu, niliendesha gari kama mwehu, nilikua na hasira sana, nilishaandika talaka tatu za kumpa mke wangu nikijiambia kuwa nikifika nampa talaka zake kisha namchukua mwanangu kwa nguvu. Nilishachoka mambo yake, mke wangu alishanifanyia ushenzi mwingi lakini kumchukua mwanangu bila idhini yake kwangu kilikua ni kitu kikubwa sana.

Mke wangu kwao ni Tanga, pamoja na kuwa yeye ndiyo aliwahi kuondoka lakini mimi ndiyo niliwahi kufika. Alichelewa kupata gari kwani hakua na tiketi na gari aliyopanda ilichelewa kujaza. Nilifika na Mama mkwe alinipokea vizuri.

“Shikamoo Baba…” Mtoto wa miaka sita alinisalimia, nilikua namfahamu kwani kama mara mbili hivi nilipoenda ukweni nilimuona. Mke wangu alinitambulisha kuwa ni mtoto wa dada yake na alikua akiishi na Mama yake, sikujali sana jina la Baba kwani kwakua nimemuoa Mama yake mdogo niliona kama ni mwanangu.

Wakati huo Mama mkwe alishatoka nnje baada ya kunikaribisha, tofauti na kwenye simu ambapo aliongea kwa kisirani tulioonana alikua mchangamfu, alinikaribisha vizuri kama vile hakuna kitu kilichotokea. Nikiwa pale simu yangu iliita, alikua ni yule rafiki yake na mke wangu amabye jana yake alinielekeza kuhusu maziwa ya kopo. Aliniulizia kuhusu mwanangu  na  kuuliza kama mke wangu alirudi. Sikuweza kuongea sana, nilimuambia.

“Niko Tanga ukweni siwezi kuongea nikitoka nitakutafuta.”

“Tanga!?”Aliniuliza kwa mshangao.

“Ndiyo kwa Mama mkwe wangu…”

“Mhhhh!” Aliguna, ni kama alikua anataka kuniambia kitu lakini alisita, nilimuuliza alikua anataka kusema nini akanyamaza na kukata simu. Wakati huo huo Mama mkwe alikua anaingia, alituuliza tunakunywa soda gani tukamtajia kisha akatuletea.

“Baba amekuja kunichukua?” Yule mtoto aliongea, Bibi yake alimkata jicho mtoto akanyamaza kimya klwa uoga, ni kama alikua anaambiwa asiropoke kitu. Kwa namna alivyonyong’onyea nilijisikia vibaya nikalazimika kumuambia kuwa nimeenda kusalimia ila wakati mwingine wakiwa likizo shuleni basi nitaenda kumchukua. Alijibu tu kukubali lakini hakua na raha.

Masaa mawili baadaye mke wangu alikuja, tofauti na nilivyodhani kuwantutagombana mpaka kufikia kumpa talaka mke wangu alinichangamkia.

“Nilijua tu utanifuata,  unanipenda sana, huwezi kuniacha, mimi nakuambia yule mbuzi ndiyo anataka tu kutuharibia lakini hawezi!” Aliongea huku akinikumbatia.

“Mambo si ndiyo haya sasa mwanangu, hakuna kugombana, mkisikiliza maneno ya wtau basi ndoa yenu haiwezi kudumu, waja ni wanafiki wanangu mambo yenu malizeni wenyewe!”

Mama mkwe aliongea, kwa namna walivyokua wamebadilika ilinishangaza sana, haikua tena mimi kumfuata mke wangu baada ya kukimbia na mtoto bali ilikua ni kama mke wangu alienda kwao kujifungua na mimi nilienda kumchukua.

“Mama inabidi tuongee, kuna mambo hayaendi sawa…” Nilimuambia Mama mkwe baada ya kukaa, sikuwalewa kabisa.

“Mwanangu haina haja ya kufufua makaburi, nimeongea na mke wako kwenye simu kanielezea kila kitu, najua wewe ni mwanaume huwezi kuomba msamaha lakini nimemuambia mwanangua kusamehe, dunia hii ni mapito tayari mna mtoto kwanini kugombana.”

Mama mkwe alinikatisha,  kila nilipotaka kuongea waliibua kitu kingine na kunifanya kushindwa kuelewana nao. Walikua wananichanganya na maneno yao.

“Hatuwezi kuondoka leo, tutaondoka kesho, Mama tutakua wageni wako sema utakaa na mtoto nataka kumuonyesha mume wangu viwanja.” Mke wangu aliniambia huku akinisogelea na kunishikashika, hakujali kama Mama yake alikua pale, alinishika sehemu mbalimbali mpaka nikaona aibu, nilikua najisogeza sogeza huku nikifurahia namna alivyokua akinishika, vidoele vyake vilinichanganya sana, nilijikuta nasisimkwa na kukosa chakuongea.

Usiku mke wangu aliniambia tutoke, alimnyonyesha mtoto tukatoka kwenda kulala nyumba ya wageni. Aliniambia kuwa kuna zawadi anataka kunipa na hawezi kunipea nyumbani kwao. Mimi niliona ninafasi nzuri ya kuongea naye kuhusiana na tabia zake kwani nilijua fika siwezi kuongea na kuelewana naye mbele ya Mama yake. Kweli tulitoka lakini hatukuongea, ile tunaingia ndani tu mke wangu alinivamia na kunipa mapenzi ambayo nilikua sijawahi kuyapata, vitu ambavyoa linipa mke wangu nilishindwa kusimulia.

Alinichanganya sana kwani niliacha kufanya naye mapenzi tangu akiwa na ujauzito wa miezi mitatu, aliniambia kuwa mimba yake hainitaki na tangu kipindi hicho nilikua sijawahi kufanya mapenzi na mwanamke zaidi ya kumalizia mambo yangu bafuni. Nilisahau kila kitu na asubuhi mimi na mke wangu tulianza safari ya kurudi tena Dar tukiwa vizuri kabisa. Maisha yaliendelea, mke wangu bado aliendelea kunywa pombe lakini hakua akichelewa kama zamani. Siku moja nikiwa chumbani nimelala mke wangu alikua sebulani, alikua akiongea na simu, kuna mtu walikua kama wanagombana naye ni kama alikua anadaiwa kitu.

Nilitoka na kumuuliza lakini hakua na jibu, alirudi chumbani kulala bila kuniambia chochote. Sikutaka kujibishana naye sana, nilirudi kulala, lakinia subuhi niliamshwa na kelele, kuna watu walikua nnje walikua wakigombana na mke wangu. Nilitoka na kukuta polisi wawili na kujana mmoja, walikua wanamuambia mke wangu kuwapa funguo za gari langu, nilienda kuulizia tatizo lilikua nini ndipo waliniambia kuwa mke wangu alikua kawauzia gari lakini kila sikua anawadanganya kuwa atawapa atawapa ila hatoi.

Nilimgeukia mke wangu kumuuliza ndipo aliniambia kuwa nikweli lakini hawezi kuwapa ufunguo kama hawammalizii pesa yake.

“Umeuza gari gani wewe? Kwani una gari?” Nilimuuliza mke wangu kwani alikua hana gari, gari pekee mule ndani lilikua ni lakwangu na lilikua na jina langu. Alinyamaza bila kujibu ndipo yule kijana alinionyesha kadi ya gari yangu na mkataba wa mauziano kuwa mke wangu alikua kapewa milioni tano ilikua badi milioni mbili, ikimaanisha kuwa mke wangu aliuza gari kwa milioni saba. Sahihi ilikua ya kwangu mke wangu alifoji sahihi yangu.

Nilimgeukia tena mke wangu na kumuuliza kama ni kweli kauza gari yangu Rav 4 New model ambayo nilinunua kwa milioni 30 ilikua hata haina maika miwili aliiuza kwa milioni saba.

“Una akili kweli wewe mwanamke, gari ya milioni 30 unauza milioni 7?” nilimuuliza kwa hasira.

“Sasa mimi kama nilikua na shida ningefanya nini, wanilipe kwanza milioni mbili zangu ndiyo niwape funguo…” Aliongea kwa nyodo.

Nilimtambua yule kijana kama John, mke wangu alikua amekuka pesa zake nyingi tu, mbali na yale makubaliano lakini mara kadhaa mke wangu alikua akienda kumkopa pesa bila kujua kuwa yuke kijana alikua akiandika na alitaka gari lake. Nilitaka kuingilia kati na kumlipa lakini alikataa na kwakua Kadi ya gari ilikua na jina langu lakini mke wangu alifoji sahihi ili kuonekana kama mimi ndiyo nilikua nimeuza ile gari. Niliangalia ule mkataba kweli ulikua na sahihi yangu, sikutaka kukubali niliikataa kabisa ile sahihi.

Kutokana na mimi kukataa basi walimkamata mke wangu na kumuweka ndani kwa kesi ya utapeli na kufoji nyaraka. Hapo ndipo nilichanganyikiwa zaidi, mke wangu alikaa kituoni kwa siku moja, nilienda kuongea na John kuona ni namna gani naweza kumlipa pesa yake aliyokua kachukua mke wangu lakini hakutaka. Aliniambia kuwa alichokua anataka ni gari, na kama siwezi kumpa basi atahakikisha kuwa anamfunga mke wangu kwakua kamtapeli pesa zake na kwakua alifoji sahihi yangu, kwamba kama mimi nikikataa kuwa ile sahihi si mimi niliyesaidi basi mke wangu anaweza kufungwa kwa kufoji.

Baada ya kuhangaika siku nzima na usiku mzima kuona namna gani naweza kulipa ile hela, asubuhi nilienda kumuona mke wangu, alikua mahabusu, nilimpelekea chai lakinia ligoma kabisa kuonana na mimi achilia mbali kula chakula nilichokua nimempelelea. Aligoma kula kwa madai kuwa nimemtelekeza kwa kitu kidogo tu, nilitaka kumuwekea dhamana lakini ilikataliwa, John alikua shatoa pesa ya kutosha hivyo nilikua napigwa chenga chenga kutwa nzima.

Mpaka wakati huo nilikua sijamuambia mtu yeyote kilichotokea, kwa kawaida nilikua sipendi kabisa kutangaza maatizo yangu. Nilihangaika sana pale lituoni lakini mke wangu hakupata dhamana, alilala tena usiku mwingine. Nyumbani sikua na amani kabisa, usiku mtoto alikua akilia, pamoja na kujitahidi sana kumpa maziwa ya dukani lakini bado alimhitaji Mama yake. Nilikaa kimya sikuwaambia ndugu zake na siku tatu nzima mke wangu alikua hataki hata kuonana na mimi.

Lakini kila siku nilikua nikienda, nilikua nikibembeleza kumuona, kuna askari mmoja wakike alikua akinisaidia mpaka kwenda kuchungulia kwenye selo alipokua, nilimuita lakini alikataa katakata kabisa kuniona mara zote akiniambia kuwa kama mimi naona kuwa Gari ni bora kuliko yeye basi nimuachea ozee jela. Alinitukana mpaka kila mtu akawa ananichangaa, nilikua kama chizi, nilijitahidi sana kutafuta pesa ya kulipa lakini John hakutaka chochote na dhamana haikupatikana na kibaya zaidi hata mahakamani hawakumpeleka.

BONYEZA HAPA UPATE MESEJI ZA MAPENZI

INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.